Historia ya Parokia

HISTORIA YA PAROKIA YA MBWENI – MT. RAPHAEL MALAIKA MKUU

Parokia ya Mbweni iko katika Mkoa wa Dar es Salaam, Wilaya ya Kinondoni, Kata wa Mbweni, Mtaa wa Mbweni Malindi Estate. Historia ya Parokia ya Mbweni inaanzia mwaka 2004, pale familia takribani 30 zilizohamia Mbweni – Masaiti kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam walipoamua kuanza kusali pamoja katika familia ya muumini mmoja Marehemu Mzee Simon Mang’ati, na baadaye kwa familia ya Ndg. Thomas Bigage. Waamini hawa waliamua kusali katika nyumba hizi kwa kuwa mahali pa kuabudia hapakuwa karibu. Kigango kilichokuwa karibu wakati huo kilikuwa Mt. Fransis wa Asizi – Mbweni lakini ilikuwa ngumu kwenda kusali huko kwa kuwa usafiri ulikuwa shida kubwa, na maeneo mengi yalikuwa mapori, hivi haikuwa rahisi kushiriki ibada Jumapili.

 

Katika juhudi zao hizo, waumini hawa wa mwanzo walifanikiwa kuunda Jumuiya mnamo mwaka 2005 na kuitwa Jumuiya ya Mt. Rafaeli chini ya Parokia ya Mwenye Heri Isidori Bakanja – Boko, wakati huo Paroko akiwa ni Pd. Ernest (2003 – 2006), Mmisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu. Ibada ya kwanza ya kuzindua Jumuiya ilisomwa na Paroko Pd. Ernest tarehe 04 Juni 2005 ikiwa na viongozi wafuatao: Melania Sangeu (Mwenyekiti); Damasi Kayanda (Makamu Mwenyekiti); Rebecca Bigage (Katibu); Lazarus Ndenji (Katibu Msaidizi); Simon Mang’ati (Mweka Hazina). Katika mazingira hayo ya ugenini (Mbweni Malindi), hakika walihitaji usimamizi wa Mt. Rafaeli msimamizi wa wasafiri, na ndivyo ilivyokuwa.

 

Jumuiya ya Mt. Rafaeli ikishirikiana na Paroko Ernest walifanikiwa kununua eneo kubwa kwa ajili ya kanisa na chekechea (kiwanja Na. 553 na 552 kwa wakati huu) na kuanza ujenzi wa kanisa la muda chini ya usimamizi wa Paroko Pd. Adolph Majeta (2006 – 2012). Wakati wote wa ujenzi ambao ulianza mwaka 2007, waamini walisali katika eneo walilokuwa wamelinunua, tena chini ya mti mkubwa, na bahati hawakuwahi kunyeshewa na mvua wala jua kuwanyima furaha ya kusali pamoja. Kwa neema za Mungu, waamini waliongezeka kwa kasi ya ajabu na jumuiya kuweza kugawanyika na kuzaa jumuiya mpya tatu yaani ya Mt. Maria de Matias, Mt. Gaspar de Buffalo na Mt. Fransis Exavery. Ujenzi wa kanisa la muda ulikamilika na kuanza kutumia kanisa hilo rasmi tangu tarehe 29/11/2009 ambapo Baba Paroko Majeta aliamua kutangaza kuwa Kigango Tarajiwa cha Mbweni Masaiti (wakati huo tukiitwa Kanda Maalum). Waamini walizidi kuongezeka na kuunda jumuiya ya tano ya Mt. Clara na ilipofika tarehe 19 February 2012, tulifanikiwa kuwa Kigango kamili cha Mt. Rafaeli – Mbweni chini ya Baba Paroko Majeta. Kuanzia mwaka huo 2012, tulipata malezi kutoka kwa Baba Paroko Pd. Dismas Mfungomali, tukiwa ni mojawapo kati ya vigango 3 vya Parokia ya Boko yaani Kigango cha Mt. Fransis wa Asizi (Mbweni Kijijini) na Kigango cha Mt. Anthony wa Padua (Mbweni Mpigi).

 

Kwa Baraka za Mwenyezi Mungu, Kigango kilijaliwa kupewa hadhi ya kuwa Parokia tarehe 6 Januari 2017 na kuweza kuwa Parokia ya 101 katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

 

UONGOZI NA MAENDELEO YA PAROKIA

Parokia ya Mbweni ilianza kuongozwa na mapadre kutoka shirika la Utangazaji Habari Njema yaani “Heralds of Good News” – HGN) kutoka India. Paroko wa kwanza na ambaye anahudumu hadi wakati huu ni Pd. Edwin Dinho (HGN). Paroko Msaidizi wa kwanza ni Pd. Sebastian Vincent (HGN). Wajumbe wa kwanza wa Kamati Tendaji ya Halmashauri ya Walei Parokia ni hawa wafuatao:

  1. Ulrich Raymond Mwinyiechi – Mwenyekiti
  2. Mathew Msechu – Makamu Mwenyekiti
  3. Mary Kasimbi – Katibu
  4. Johnson Mshana – Katibu Msaidizi
  5. Mhazini – Philipo Mushi

Viongozi hawa ndio wanaoongoza Halmashuri ya Walei Parokia hadi sasa isipokuwa Ndg. Mathew Msechu ambaye alibadilishwa kutokana na majukumu mengi na akachaguliwa Ndg. Theonest Mutegeki ambaye anahudumu hadi wakati huu.

 

Parokia ya Mbweni ina jumla ya waamini 1300 ambao wanatoka katika Jumuiya 9 za sasa ambazo ni Mt. Raphael; Mt. Maria de Matias; Mt. Gaspar del Buffalo; Mt. Fransis Exavery; Mt. Maximillian Kolbe; Mt. Clara; Mt. Clement; Mt. Inyasi wa Loyola na Mt. Joseph Mfanyakazi. Parokia pia ina VMJ 7 ambavyo ni Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu (VIPAPA); Vijana Wafanyakazi Wakatoliki (VIWAWA); Umoja wa Kwaya Katoliki Tanzania (UKAKATA); Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu; Karismatiki Katoliki; Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA); Umoja wa Wanaume Katoliki (UWAKA).

Hakuna taasisi za kikatoliki ambazo ziko chini ya parokia. Hata hivyo, Parokia imefanikiwa kununua viwanja viwili  zaidi yaani Na. 535 na Na. 550 kwa ajili ya matumizi ya hospitali na biashara hasa ya benki na juhudi zinaendelea kuendeleza maeneo hayo. Parokia imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa nyumba ya Mapadre na sasa tuko katika hatua za mwisho kuanza ujenzi wa kanisa la kudumu kama linavyoonekana kwenye picha pembeni.

 

TUMSIFU YESU KRITU.